23 September 2017


RAIS wa Zanzibar na Mwenyeki wa Baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, ametangaaza kufuta michango ya elimu ya sekondari, kwa skuli za serikali kuanzia mwezi Julai mwaka 2018, na kuitaka wizara ya fedha kuiangalia upya bajeti kuu ya Wizara ya elimu Zanzibar.
Alisema uwezo huo serikali unao, bila ya kuomba ufadhili kutoka kwa wafadhili wa nje ya nchi, kama ilivyofanya kwa kufuta michango kama hiyo kwa elimu ya msingi, hivyo nayo ya sekondari itafutwa kuanzia mwakani.
Dk Shein, ameeleza hayo uwanja wa wa michezo Gombani Chakechake kisiwani Pemba, wakati alipokuwa akizungumza na mamia ya wanafunzi, wazazi, wananchi na watendaji wengine  wa serikali, kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka ya 53 ya Mapinduzi yaliofanyika kisiwani Pemba kitaifa.
Alisema kwa vile muasisi wa taifa hili, alitangaaza elimu bila ya malipo miaka 53 iliopita, sasa lazima na serikali anayoiongoza itekeleze hilo kwa vitendo, ndio maana alianza kwa elimu ya msingi na sasa kuanzia mwakani, ni kwa elimu ya sekondari.
Alisema anaamini bejti kuu ya wizara ya elimu, inatosha kugharamia elimu ya sekondari, na ndio maana akaiagiza wizara ya fedha kuiangalia tena upya bajeti ya wizara ya elimu ya mwaka wa fedha 2018/2019.
“Na michango ya elimu ngazi ya sekondari nayo natangaaza kuifuta kuanzia tarehe 1/7/2018, kama nilivyofuta michango ya elimu ya msingi kwa skuli zote za serikali”,alisema.
Akizungumzia kuhusu ubora wa elimu, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, alisema serikali inaendelea kuimarisha pia majengo kwa kuzifanyia matengenezo na upanuzi wake.
Alisema, serikali inampango wa kujenga skuli tisa za ghorofa kwa Unguja na Pemba, skuli 23 kufanyiwa upanuzi na kuongezwa vyumba vyengine vya madarasa, kuweka samani, ujenzi wa maabara ya sayansi na ununuzi wa vitabu.
Alifafanua kuwa, aidha jengine katika kuimarisha sekta ya elimu, serikali itaendelea kukabiliana na changamoto nyengine mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha maslahi ya waalimu kwa kulipa malimbikizo yao mbali mbali.
Hivyo, ameiagiza wizara ya elimu, kuhakikisha wanalifuatilia hilo kwa haraka, ili waalimu wafanye kazi zao kwa ufanisi kama walivyowafanyakazi wengine wa sekta ya umma.
“Naamini, niliongeza mshahara ya watumishi wa umma kutoka shilingi 150,000 hadi shilingi 300,000 ambapo naamini na waalimu wakiwa kama watumishi wa umma, nao wamefaidika na hilo”,alifafanua.
Aidha amewataka waalimu hao kuendelea kufanya kazi zao kwa kufuata maadili, kanuni na sheria za utumishi za uuma, ili watoe elimu kwa ufanisi wawapo madarasani.
Alisema waalimu ndio kioo cha jamii, hivyo lazima hilo walielewe kwa kufanyaka kazi zao vyema, ili wazalishe wanafunzi bora waliojaa elimu.
Katika hatua nyengine, Rais huyo wa Zanzibar, amewataka wazazi na walezi, kuendelea kufuatilia nyenendo za watoto wao, ili kuhakikisha wanafika madarasani.
Alisema wazazi hao wanaomchango mkubwa, katika kufanikisha ubora wa elimu nchini, kwa kule kuwaharakisha watoto wao, kwenda skuli sambamba na kuwataka wadurusu masomo yao.
“Wazazi na nyinyi lazima tuungane pamoja na waalimu, katika kufuatilia nyenendo za watoto wenu, kwa kuwakumbusha kudurusu masomo na lazima muhakikishe wanafika masomoni kwao”,alifafanua.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe: Riziki Pembe Juma, alisema sherehe hizo za elimu bila ya malipo zilizoamshwa na Rais wa Zanzibar, zimerejesha umoja na mshikamano miongoni mwa waalimu, wanafunzi na watendaji wa wizara yake.
Alisema sherehe hizo ambazo miaka ya 2000 zilionekana kusuasua, na sasa kuibuliwa upya kwa mawazo ya rais wa Zanzibar, yameirejeshea heshima wizara ya elimu kwa kuendelea kuibua vipaji vya kimichezo.
Mapema Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khadija Bakar Juma alimpongeza rais huyo wa Zanzibar kwa kufuta michango ya elimu kwa wanafunzi wa skuli za serikali.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo aliwataka wazazi na walezi kuwaandikisha watoto wao skuli ya msingi, kwani hakuna michango yoyote skulini hapo baada ya kufutwa na rais wa Zanzibar.

Awali rais huyo wa Zanzibar alipokea maandamano ya wanafunzi wa mikoa  mitano ya Zanzibar, yalioanzia nje ya uwanja wa Gombani, na kisha kukabidhi zawadi kwa washindi wa michezo, huku mshindi wa jumla ukiwa ni Mkoa wa kusini Pemba ambapo walikadhiwa kikombe na Rais wa Zanzibar.

About Me:

My Name is Hussein H. Hussein, I am a Journalist by proffessional, dealing with Radio and TV Braodcastin, News Gathering and Writting, Creating Radio and TV adverts, Producing Radio and TV programs, Events Coverage, Editing Visual and Audio Contents, Shooting, Photography, Graphic designing and Social Media Contents


Connect With Me: TWITTER | FACEBOOK | GOOGLE PLUS

Newer Post
HABARI ZILIZOPITA
Habari Mpya Zilizopita