MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar
Khamis Othman amesema, katika kutekeleza agizo la rais wa Zanzibar Dk: Ali
Mohame Shein kuhusiana na walimu watoro, ameanza kwa kupata orodha ya walimu
wote wa mkoa wake, ili iwe rahisi wakati atakapofanya ziara za ghafla skulini,
kuwatambua.
Akizungumza
na Zanzibarleo Ofisini kwake Wete alisema, watahakikisha maagizo yote
yaliyotolewa na Rais wanayatekeleza ipasavyo likiwemo hilo la waalimu watoro.
Alisema kuwa,
walimu hao atawafuatilia kwa kuwapitia katika skuli zao wanazosomesha bila ya
kutoa taarifa, ili kuweza kuwabaini walimu wenye kufanya tabia ya utoro.
“Tutakwenda
skuli zote kimya kimya na tukifika tu tunazichukua simu za za walimu waliopo,
ili wasije wakawapigia”, alisema Mkuu huyo.
Mkuu huyo
alieleza kuwa, watazifuatilia skuli moja baada ya moja na endapo watabaini kuna
walimu wenye tabia hiyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Ikiwa
mwalimu ana matatizo basi tupate taarifa yake kamili, lakini kinyume na hivyo
tutamchukulia hatua za kisheria”, alieleza.
Aidha
alieleza kuwa, pia watahakikisha wanapeleka miundombinu ya maji maskulini, ili
kuondosha tatizo hilo lililopo kwa baadhi ya skuli, kwani yote yamo katika
mkakati wa kufanyia kazi.
Akizungumzia
agizo jengine kwa soko la Tumbe Wilaya ya Micheweni Pemba, Mkuu huyo alisema,
soko hilo lipo kwenye matengenezo, ambapo ndani ya miezi miwili litaweza
kutumika.
“Sasa hivi
wanasubiri huduma ya maji safi na salama, ili waingie ndani ya soko, hivyo
tutahakikisha ndani ya miezi miwili wafanyabiashara wetu wataingia ndani ya
soko hilo”, alisema Mkuu huyo.
Hayo ni
miongoni mwa maagizo aliyoyatoa Raisi wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein katika mkoa huo ili yatekelezwe, ambapo tayari
maagizo yote yamo katika mkakati wa kufanyia kazi.