WASAIDIZI wa sheria wanaoendelea na
masomo yao, kwenye Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba,
wametakiwa kuyachukua kwa umakini mkubwa mafunzo wanayopewa, ili wapate
kuisiadia jamii kwa uhakika na sio kubabaisha.
Kauli hiyo,
imetolewa na Mratibu wa Kituo hicho Fatma Khamis Hemed, wakati alipokuwa
akifungua mafunzo ya siku mbili, kwa wasaidizi hao wa sheria, juu ya
kukumbushwa sheria mbali mbali, ambazo wanapaswa kuielimisha jamii.
Alisema msaidizi
wa sheria bora, ni yule anaefanyakazi zake kwa umakini na baada ya kupewa
mafunzo ya kisheria kuyasikiliza vyema na kisha kuifundisha jamii yake, na
kinyume chake ataendelea kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema
pamoja na kwamba wasaidizi hao wa sheria wanadarasa yao kila mwisho wa mwezi,
juu ya masomo mbali mbali, lakini pia mafunzo kama hayo ya siku mbili, wakiwa
makini wataongeza uwelewa wa kazi zao.
“Mafunzo
haya ya kuwakumbusha nyinyi sheria mbali mbali kama ya ushahidi na ile ya
maendeleo ya karafuu, mkiwa makini mtatoa msaada wa kisheria vyema kwa
jamii”,alifafanua.
Katika hatua
nyengine Mratibu huyo, aliwataka wasaidizi hao wa sheria, kuendelea kujisomea
mambo mbali ya kisheria, ili waongeze ufanisi kwenye kazi yao ya kuihudumia
jamii.
Mapema Mratibu
wa mafunzo hayo Safia Saleh Sultan, alisema wasaidizi wa sheria, wanalojukumu
la kuwasaidia wananchi juu ya mambo kadhaa ya kisheria, hivyo mafunzo na
taaluma wanazopewa ndio dira.
Akiwasilisha
mada ya haki za wanawake kwa mujibu sheria, alisema wanayohaki ya kupewa elimu,
kusikilizwa, ajira na nafasi ya uongozi kama walivyo wanaume.
“Mwanamke
anatambulika kisheria kuwa nae anapaswa kupewa haki na fursa sawa na mwanamme,
na pia yapo matamko mbali mbali yaliochapuzi hilo, likiwemo la kimataifa la
haki za bidamu”,alifafanua.
Mapema
wakili wa serikali kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashitaka kisiwani Pemba, Juma
Ali Juma, alisema sheria mpya ya ushahidi no 9 ya mwaka 2016, baada ya kufutwa
ile ya mwaka 1917, sasa inatambua ushahidi wa kieletroniki.
Alieleza
kuwa, sheria hiyo kwa sasa pia inaukubali ushahidi wa mtoto au mtu mwenye ulemavu
wa kutozungumza, jambo ambalo hapo kabla hilo halikukubalika.
“Jamii
lazima muielimisha kuwa, sheria mpya ya ushahidi, sasa imeimarishwa suala la
ushahidi , hivyo wasiwe na mashaka iwapo kuna mtoto kabakwa na hakuna mtu
mwengine alieshuhudia”,alifafanua.
Baadhi ya
washiriki wa mafunzo hayo, walisema bado jamii inahitaji elimu kwa upana zaidi,
maana kesi nyingi hufutwa na mahakama kutokana na mashahidi kutohudhuria.
Walisema,
jamii inadhani kesi zote zinazofutwa mahakamani, hutokana na mahakimu na
waendesha mashitaka wamekula rushwa, ambapo wakati mwengine huwa sio sahihi.
Katika
mafunzo hayo ya siku moja, mada kadhaa zilijadiliwa, ikiwa ni pamoja na sheria
ya kuwalinda wari na watoto wa mazazi mmoja no 4 ya mwaka 2005, sheria ya mtoto
no 6 ya mwaka 2011, sheria ya ushahidi no 9 ya mwaka 2016, sheria ya Maendeleo
ya karafuu ya mwaka 2014 na kanuni yake.